Morogoro
ilivyogubwa, mapigano wakulima na wafugaji tangu 1955
Na
Thadei Hafigwa
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli aliwaahidi
watanzania kuwa atahakikisha anaipatia ufumbuzi migogoro ya wakulima na
wafugaji iliyoshimiri katika maeneo mbalimbali hapa nchini ambayo
inatahatarisha amani na utulivu hapa nchini.
Ahadi
hizo Dk.Magufuli alizitoa wakati wa kampeni wa kusaka nafasi ya kushika
dola mwaka jana na hata baada ya kufanikiwa kuingia Ikulu ya Magogoni
kiasi cha kupelekea kuanza kuchukua hatua za awali wakati akifanya
uteuzi wa wakuu wa mikoa hivi karibuni,ambapo moja ya kigezo
alichokitumia kwamba asingeweza kumteua mtu kushika nafasi hiyo iwapo
eneo lake alishindwa kuipatia ufumbuzi mgogoro wa wakulima na wafugaji
Mkoa
wa
Morogoro ni miongoni mwa mikoa iliyogubikwa na changamoto kubwa ya migogoro ya
wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikipewa tafsiri mbalimbali na hata kuhusisha
na baadhi ya viongozi serikali kwamba walichangia kushamiri kwa uwepo wake kwa
namna moja au nyingine.
Wahanga wakuu wa migogoro
hiyo ni wananchi wa kada ya chini kwa kile kinachoelezwa kuwa historia ya
migogoro hiyo ambayo imeanza toka mwaka 1955 baada ya jamii ya wafugaji kuingia
katika mkoa wa Morogoro hususan wilaya ya Kilosa wakitokea maeneo ya Manyara na
Arusha.
Vyanzo mbalimbali vya habari kiwemo taarifa za kiserikali
zinaonesha ya kuwa mgogoro wa kwanza ulitokea mwaka 1955 katika kitongoji cha
Italagwa,kata ya Iyogwe ambapo kiini chake ni wafugaji kuwalazimisha wakulima
wahame bonde walilokuwa wakilitumia kwa kilimo.
Kutokana na mgogoro huo
yalipelekea kutokea mapigano ambapo baadhi ya wakulima na wafugaji walipoteza
maisha, mali nyingi kuharibiwa yakiwemo mazao, nyumba kuchomwa moto na kuacha
wajane na majeruhi wengi.
Kama hiyo haitoshi,
kumbukumbu pia zinaonesha ya kuwa juni 4, 1967 katika kata ya Chakwale
yakaibuka mapigano mengine, baada ya kijana kutoka jamii ya wafugaji(morani)
kumzuia mkulima aliyefahamika kwa jina moja Chisanza asiuze ng’ombe kwenye
mnada,inadaiwa mkulima huyo alipigwa na kuujeruhiwa.
kwa wakati huo,Silaha za kijadi
zilitumika, mishale kwa upande wa wakulima,huku kwa upande wa wafugaji
wakitumia sime,marungu na fimbo “mapigano yaliendelea kwa siku tatu,yalienea
eneo lote la kuguru kutokana na
kugubikwa kwa chuki na manyanyaso baina ya pande zote mbili.”ni sehemu ya
taarifa za kiserikali zilizopatikana wilayani Kilosa.
Pia mwaka 1975 kulitokea
mapigano baina ya wakulima na wafugaji maeneo ya Magole na Madudu maeneo ambayo
jamii ya wafugaji walihamia kutoka Gairo na Chakwale ambapo chanzo cha tukio
hilo ni vijana kutoka jamii ya wafugaji kulisha mifugo yako kwenye mashamba ya wakulima yalikuwa na mazao
yaliokuwa mashambani.
Kufutatia tukio hilo,watu
12 walikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na hatimaye waliachiwa
huru na mahakama.
Septemba,Mwaka 1979 yalitokea mapigano mengine katika Kijiji cha Rudewa, tarafa ya Kimamba
chanzo hakikuwa tofauti na matukio yaliotangulia kiini ni vijana wa jamii ya
wafugaji kulisha kwenye shamba la mikunde la mkulima mmoja aliyefahamika kwa
jina la Jabili ambapo katika tukio hili liligharimu maisha ya wakulima wanne na
wengine wawili walijeruhiwa.
Silaha za jadi na bunduki zilitumika katika
mapingano hayo.
Hali hiyo haikoma,
iliendelea ambapo ilipofika desemba 8, 2000 hali ya mapigano ilijirudia katika
kijiji cha Rudewa, Wilayani Kilosa, wakulima 32 waliuawa, silaha za moto
(bunduki) zilitumika katika mapigano ambapo zipo taarifa kwamba baadhi ya
wafugaji walitoka nje ya Mkoa wa Morogoro kuongeza nguvu ya mapigano hayo.
Tukio
hili liliacha Wajane 7 walemavu 8 yatima 10, na watu kukoosa makazi baada ya nyumba
61 kuchomwa moto.
Mwaka mmoja baadaye, mwaka
2001 mapigano yalizuka tena katika kijiji cha Chogoali,kitongoji cha Masimbani
kata ya Iyogwe, wafugaji waliwalazimisha wakulima waondoke kwenye bonde ili wao
wafugie mifugo yao.
Oktoba 27, mwaka 2008
kukazuka tena mapigano ya wakulima na wafugaji katika kitongoji cha Kikenke,kijiji
cha Mamwegwa,kata ya Msowero huko wilayani Kilosa, ukiacha matukio hayo ya
mapigano pia kuna kesi nyingi za wafugaji na wakulima zimekuwa zikiripotiwa
kwenye mamlaka mbalimbali huku wadau,wanaharakati,viongozi wa dini,na serikali
ikijaribu namna ya kutafuta suluhu ya kumaliza migogoro hiyo.
Mkuu
wa Wilaya ya Kilosa
Mkuu wa Wilaya ya
Kilosa,John Henjewele alisema kiini cha kuwepo kwa migogoro ya wakulima na
wafugaji hususan kwenye eneo lake la utawala linatokana na kutokuwepo kwa
matumizi bora ya ardhi ambapo suluhisho pekee ni kupima upya ardhi ili wafugaji na wakulima waweze kuishi bila
ya kuingiliana katika shughuli za uzalishaji mali.
Henjewele alibainisha
kwamba halmashauri ya wilaya ya Kilosa imechukua hatua ya kupiga marufuku
uingizaji wa mifugo mipya katika halmashauri hiyo kwa lengo la kutaka kujua
mahitaji halisi ya wafugaji waliopo wilayani humo ili serikali ya awamu ya tano
iweze kuipatia ufumbuzi wa kudumu.
Aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa
Morogoro Dk.Rajabu Rutengwe ambaye hivi karibuni alitoa taarifa yake wakati wa
mabidhiano na ofisi kwa mrithi wake,Dk Steven Kebwe kwamba changamoto kubwa za
Mkoa ni Migogoro Sugu ya wakulima na wafugaji yenye umri zaidi ya miaka 34.
Idadi ya matukio ya
mapigano na mauaji baina ya wakulima na wafugaji, tangu alipoingia mkoani
humo katika nafasi ya ukuu wa Mkoa kwa miezi 14 iliyopita hayakuwepo hadi Desemba,
2015 na Februari, 2016.
“Hakika matukio haya matatu
yote yamekuwa ya ghafla na Serikali tumechukua hatua. Migogoro hii inakabiliwa na rushwa, mifugo
mingi kuliko uwezo wa ardhi, Polisi idara ya upelelezi kutowajibika kwa wakati,
Mahakama kuhujumu baadhi ya kesi za mauaji ya wakulima, watendaji na viongozi
ngazi za chini na wanasiasa kuhusika”alisema.
Aidha, taarifa za
intaligensia zinaashiria baadhi ya mifugo ya watu mashuhuri kutoka Mikoa ya
Arusha, Manyara, Shinyanga na Simiyu ambako malisho yamemalizika, wamekuwa
wanalazimisha kuingia mkoani Morogoro bila ya utaratibu.
Kiini cha mgogoro
wa wakulima na wafugaji ni nini?
Dk Rutengwe anasema “ukiniuliza
migogoro hii kiini chake ni nini? Jibu
ni uanzishwaji maeneo ya kiutawala bila ya kufuata sheria na taratibu, aidha
maeneo haya mapya yakapora ardhi kubwa kutoka vijiji mama. Uongozi wa Vijiji mama na majirani
kutokuridhika na kupigania haki zao hadi kufa”
Kuhusu Mgogoro sugu wa wakulima
na wafugaji katika eneo la Mabwegere ambapo kiini cha mgogoro kati ya wakulima
na wafugaji Dk.Rutengwe alifafanua kuwa ni uanzishwaji maeneo ya kiutawala bila
ya kuzingatia sheria, jukumu hilo alikabidhiwa Mzee Stephen Mashishanga kama
msuluhishi baada ya msuluhishi wa awali Mzee Paul Kimiti kujitoa kwa kile
kinachodaiwa kuona ugumu na historia ya mgogoro huu.
Miezi
14 ya Dk.Rajabu Rutegwe Morogoro
Tukio la kwanza 11.12.2015
tangu kuwa Mkuu wa Mkoa Morogoro, kundi la ng’ombe 162 lilionekana kula shamba
la kunde nusu ekari ambapo mkulima Bakari Ramadhani na wenzake wakawachukua
ng’ombe hao mpaka Ofisi ya Kijiji cha Dihinda na kuwalinda hadi Desemba 12,2015,
ambapo Shabani Itel alifika na kudai ng’ombe hao ni mali yake na kukubali kulipa kiasi cha
shilingi laki mbili (200,000/=) kama fidia ya uharibifu.
Mkulima Mohamed Mussa (43)
alifariki dunia baada ya kuchomwa mkuki tumboni na wafugaji jamii ya
Wamang’ati, wakati analinda ng’ombe zilizokuwa zimekamatwa na wakulima kwa kosa
la kulisha shamba la Kunde la mkulima Bakari Ramadhani. Baada ya kurupushani wakulima waliwakatakata
ng’ombe 155 na kuwaacha wamelala chini.
Tarehe 14.12.2015 wakati
wa ufuatiliaji wa tukio la mauaji kumbukumbu na MBW/IR/901/2015 ilibainika
Askari mmoja, alizingirwa na jamii ya wafugaji na kurushiwa mkuki ndani ya gari la Polisi.
Hatua
zilizochukuliwa:
Polisi ikiongozwa na Mkuu
wa upelelezi Wilaya ya Mvomero walikesha katika eneo la tukio ambapo watu 19
walikamatwa katika tukio hili. Kutokana
na uzito wa vurugu hizo Polisi ziliongeza nguvu katika eneo la tukio.
Tukio la pili 14.12.2015
Ni
ugomvi wa ardhi uliotokana na kugombania mipaka ya mashamba kati ya wakulima na
wafugaji katika kitongoji cha Tindiga. Jamii ya wafagaji wanadaiwa
kushirikiana na mabepari wa ardhi
maarufu “meza meza” eneo la Tindiga. Wakiwemo viongozi wa Serikali ya Kijiji na
wafanyabiashara.
Madhara:
Eneo la Ruhoza mashambani
Kijiji cha Tindiga, Tarafa ya Masanze, wilaya ya Kilosa. Mafugaji wanaokadiriwa 60
walivamia wakulima kutoka Kijiji cha Tindiga B waliokwenda kuoneshana mashamba
ili kutambuliwa na Serikali ya Kijiji.
Wakulima 8 walijeruhiwa.
Hatua
zilizochukuliwa:-
Watuhumiwa 2 jamii ya
Kimasai walikamatwa. Kamati ya Ulinzi na
usalama mkoa ilifanya mazungumzo na wananchi na kuelekeza Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Wilaya na Halmashauri kutatua mgogoro wa mipaka katika eneo husika.
Tukio
la tatu 09.02.2016
Wafugaji
walilisha mifugo kwenye shamba la mpunga ekari 1, mali ya mkulima mmoja mkazi wa Kijiji cha Dihombo.
Madhara:
Kutokana na hasira kundi la watu wajulikanao “Mwano”
lilivamia mifugo ya mfugaji Nuru Kapande na kuua mbuzi (27), Kondoo
(8), Ndama (3) na kujeruhi mbuzi (22) Kondoo (19) na ndama (1).
Hatua
zilizochukuliwa:
Watuhumiwa 21 walikamatwa
na kufikishwa mahamani kwa kosa la kujeruhi wanyama.
Wadau
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Morogoro Innocent Karogesi akielezea juu ya suluhisho la Mgogoro wa wakulima
na wafugaji aliwataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuendesha
sensa maalum ya kujua idadi ya mifugo na pia kuangalia namna ya kuwaweka alama
maalum mifugo iliopo kwenye halmashauri
zao ambayo itofautishe kati halmashauri moja na nyingine ili kuweza kubaini
mifugo mipya.
Wafugaji
Mwenyekiti wa Kijiji cha
wafugaji Parakyo,Wilayani Kilosa,Palakoris Koligi alisema suala la amani baina
ya wakulima na wafugaji ni jambo la msingi sana lakini kinachopelekea kutokea
mgogoro wa wakulima na wafugaji ni kukosekana na kwa malisho ya kutosha pamoja
na maji kwa ajili ya kunywesha mifugo katika vijiji vya wakulima.
Koligi alisema ni jukumu
la serikali ya awamu ya tano kuandaa mazingira rafiki kwa wafugaji ili
kuhakikisha majosho na malambo(mabwawa) yanajengwa katika maeneo ya wafugaji
ili kuepusha migogoro hiyo kwa kile alichokieleza kwamba wanalazimika kutafuta
maji ndipo wanapojikuta wanaharibu mazao ya wakulima na mgogoro unazuka.
Wakulima
Mmoja wa wakulima
aliyehojiwa na mwandishi wa makala hii,Gervas Mtitu alisema mgogoro wa wakulima
na wafugaji hauwezi kwisha iwapo wafugaji hawataacha kuchungia kwenye mashamba
ya wakulima.
Pia alitoa angalizo kwa
baadhi ya wakulima wenzake
wanaoshirikiana na na baadhi ya wanasiasa katika ngazi ya kata na wilaya kuacha
kuuza ardhi kilolela bila ya kufuata sheria
hali hii inachangia kuzuka kwa migogoro ya wakulima na wafugaji na
kukiuka matumizi bora ya ardhi
Dk.Steven
Kebwe
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Dk.Steven
Kebwe aliyeteuliwa hivi karibu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nafasi
ya ukuu wa mkoa alionesha dhamira yake ya kupambana na migogoro ya wakulima na
wafugaji katika mkoani humo kufuata misingi iliyoandaliwa na kamati za ulinzi
na usalama katika ngazi za wilaya na mkoa kwa kuwa ni nzuri isipokuwa zilikosa
usimamizi na ufuatiliaji wa karibu.
Dk.Kebwe alijinasibu kuwa
kuteuliwa kwake kuwa mkuu wa Mkoa wa Morogoro kufanya kazi za siasa bali
kufanya kazi za kiserikali na kuchukua hatua kwa wale wote ambao watabainika
kuwa chanzo cha kushamiri kwa mgogoro wa wakulima na wafugaji.
Hata hivyo,hatua za
mashauriano inahitajika bila kuegemea upande mmoja ili kuhakikisha
ya kuwa Mkoa wa Morogoro unabaki kuwa salama na mipango ya kuleta maendeleo kwa
wananchi inakamilika kwa wakati.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0754683186,e-mail hafigwa@yahoo.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni